NA GORDON KALULUNGA
TAKRIBANI wiki mbili sasa, kumekuwa na matamko mbalimbali kutoka kwa baadhi ya viongozi wa dini kuhusu suala la kupigia kura rasimu ya Katiba “penyezwa” ambayo imeandikwa neno pendekezwa.
Baadhi wanasema ukifika wakati wa kupiga kura, waumini wao wapige kura ya hapana, wengine wanasema waumini wao kila mmoja atumie akili yake, iwe Ndiyo au Hapana.
Sijamsikia hata mmoja akisema kuwa anatenga muda wa kuwaelimisha waumini wake kuhusu rasimu hiyo ubaya au uzuri wake, hapa najawa na shaka kuwa yawezekana hata wanaotoa matamko baadhi yao pia hata hawajaisoma.
Wakati natafakari matamko hayo na mahubiri kutoka katika baadhi ya nyumba za ibada ambazo tunaamini kuwa ni tulizo ya mihemko ya mioyo yetu huku imani ikiwa ni kutupeleka Mbinguni, ni kwamba natamani kwenda katika nyumba hizo za ibada na wakati ibada ikiendelea, waruhusu maswali.
Kama itakubalika, watoa matamko ambayo kimsingi yanalenga manufaa ya kisiasa, waruhusu nasi tuwahoji baada ya mahubiri yao kwa sisi waumini wao ili wajipime kama wapo sahihi au la!
Suala hili linanikumbusha mambo mawili, mosi ni suala la Mchungaji Kibwetele wa Uganda, ambaye alihamasisha waumini wake wauze mali na kisha kujifungia kanisani na kuchomwa moto huku yeye akiukimbia moto na kuikimbia nchi na hapo naikumbuka pia kauli ya Rais Jakaya Kikwete kuwa akili za kuambiwa changanya na zako.
Nipende kumpongeza Rais Kikwete kwa uamuzi mgumu wa kuchukua hatua ya kuandika Katiba Mpya ambapo alisema kuwa, kama wananchi wataikataa, itaendelea kutumika iliyopo sasa.
Halazimishi rasimu hii kupitishwa na kuanza kutumika, bali amewaachia wananchi waamue.
Niwapongeze pia wabunge na wajumbe wateule waliokuwa ni moja ya jopo la kwanza mbali na baadhi kususia, lakini nawapongeza wote kwasababu hakuna hata mmoja ambaye hakuchukua posho ambazo ni jasho la watanzania wote.
Posho hizo ambazo kwa siku walikuwa wakichukua ni sawa na mshahara wa mtumishi wa umma kwa mwezi au daftari 3000 za wanafunzi wa shule ya msingi ya serikali huku nyikani.
Nilipojaribu kuisoma Katiba hiyo inayopendekezwa na kuwashirikisha watu wengine wa huku nyikani, hakika jasho lilinishuka.
Sihamasishi wananchi wenzangu wenye uelewa watakavyosoma au kusomewa, au kuelezwa, au kuhamasishwa, au kushika yale watakayoambiwa na viongozi wa vyama vyao vya siasa na dini zao kuwa wapigie kura ya ndiyo au hapana, bali nahamasisha kila anayejua kusoma na kuandika aisome vema Katiba hiyo inayopendekezwa.
Katika ukurasa wa 1 na ule wa 2 sehemu ya Kwanza yenye maandishi makubwa yasemayo Jina, Mipaka, Alama, Lugha na tunu za Taifa, kipengee cha kwanza na cha pili kinaacha maswali mengi na yawezekana baadae tukampata Rais anayeweza kuiingiza nchi yetu katika machafuko kwa kuvamia nchi zingine.
Vipengele hivyo vinasema, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi yenye mamlaka kamili ambayo imetokana na Muungano wa nchi mbili za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya watu wa Zanzibar ambazo kabla ya Hati ya makubaliano ya Muungano ya tarehe 22 Aprili, 1964 zilikuwa nchi huru.
2.(1) Eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni;
(a) eneo lote la Tanzania Bara, ikiwa ni pamoja na eneo lake la bahari ambalo kaba ya Muungano lilikuwa likiitwa Jamhuri ya Tanganyika pamoja na maeneo yote yatakayoongezeka; na
(b) Eneo lote la Zanzibar, ikiwa ni pamoja na eneo lote la bahari ambalo kabla ya Muungano lilikuwa likiitwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar pamoja na maeneo mengine yatakayoongezeka.
Swali akilini linakuja kuwa hayo maeneo yatakayoongezeka kwanini hayawekwi wazi? Yatatoka wapi? Ni swali dogo sana kwa watawala lakini linazua mkanganyiko kwa baadhi ya watu wa huku nyikani.
Katiba hiyo ukurasa wa 18 na 19 ambapo ipo sura ya tatu na kueleza suala la Ardhi, maliasili na mazingira, inasomeka kuwa (a) raia wa Tanzania pekee ndiye atakayekuwa na haki ya kumiliki ardhi ya Tanzania, na haki hiyo italindwa kwa mujibu wa Katiba hii;
(b)mtu ambaye siyo raia wa Tanzania atakuwa na fursa ya kutumia ardhi kwa ajili ya uwekezaji na maendeleo mengine ya kiuchumi na makaazi.
Sasa hapo sijui mtu anayetaka kujenga ama kutumia makazi anakuwa na hati au anajenga tu vyovyote, hapa najikita kutafuta uelewa kabla ya kupiga kura ya Ndiyo au Hapana.
Kwa nchi hii ninavyofahamu ni kwamba Katiba hiyo inayopendekezwa, serikali kama itashupalia kuwa lazima watanzania tuingie katika suala la kupiga kura, basi haina haja ya kupoteza fedha maana itapita tu.
Lakini naomba niwakumbushe wasomaji wangu kuwa, niliwahi kuandika haya yafuatayo katika safu hii.
‘’Nitailinda na kuitetea Katiba ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania’’ hiki ndicho kiapo alichokiapa Rais Jakaya Mrisho Kikwete alipokuwa akiingia madarakani.
Nilisema, Watanzania walikichagua Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuendelea kuongoza dola kutokana na ilani ya chama hicho na mwelekeo wake.
Katika ilani ya chama hicho 2015-2025, hakuna mstari wowote ambao umeeleza kuwa CCM ikiingia madarakani itaanzisha mchakato wa Katiba mpya.
Sina uhakika kama Kamati kuu au Halmashauri kuu ya CCM, kama ilimhoji Rais Kikwete ambaye ametuleta ilani ambayo haipo kwenye maandishi ya chama madhubuti, CCM.
Kuna dalili za ilani ya Kikwete kuhusu Katiba mpya kukataliwa na wananchi, kama vikao havikuipitisha na itakuwa aibu kwake na chama chake.
Iliwahi kutokea aibu ya mpango Oparesheni tokomeza ujangili, Kimbunga na tuendako naiona ‘’Oparesheni’’ Big Result Now(BRN).
Mpango ambao unaonesha matunda chanya ni Shule za sekondari za kata.
Hakuna ubishi kuwa watu wengi wanaogopa mabadiliko.Watu wa nyikani, wanasema, eti tangu awali walishangazwa na uteuzi wa Rais Kikwete kumteua Jaji Warioba kuwa Mwenyekiti wa tume hiyo!
Watu wa nyikani wanatamani kuwa na katiba ya kutukutanisha wakati wowote, kwa jambo lolote linalohusu utaifa wetu, lakini hawana uhakika kama hii na ile ya awali ya Jaji Warioba kuwa ndiyo Katiba inayotafutwa.
Wanakumbuka kuwa eti, hivi karibuni, kuna baadhi ya vyombo vya habari vilimnukuu Jaji Warioba akiwasihi wabunge wa bunge la katiba kuwa wasiyaondoe yale aliyoyaandika kwenye rasimu yeye na wenzake.
Kauli yake haikuwasikitisha watu wa nyikani kwasababu eti ilionesha ni jinsi gani alijaa hofu ya kuondolewa yale yanayodhaniwa kuwa ni mawazo yake yaliyomo kwenye rasimu.
Kuna wakati nilitumwa na Bibi na shangazi kumweleza jambo Jaji Warioba kuwa waliwasikia baadhi ya watu wakisema eti, katika Rasimu, maoni mengi yaliyoandikwa yalikuwa ni yake na wasiomtakia mema Rais Kikwete na Muungano.
Hayo yalikuja kutokana na mawazo yaliyokusanywa mwanzo kuungwa mkono na watu wa upande wa pili na ndiyo yalitaka kumkosanisha na ‘’mke’’ wake wa kwanza(CCM).
Shangazi mpaka sasa anazidi kusisitiza na kukumbusha kuwa, Warioba asikate tamaa, ila asisahau kuwa eti baadhi ya watu hawasahau historia.
Baadhi ya watu wanahisi eti Jaji amehama nayo yale aliyowahi kuyasema awali, wakati yeye Jaji anasema ni mawazo ya sasa na siyo yake bali ni ya watu ingawa naye wakati ule aliwahi kuwa na mawazo kama hayo na aliwahi kuyatamka.
Kwa sasa kinachotakiwa, viongozi wa dini waachane na matamko waliyoyatoa, kwasababu Katiba inayopendekezwa, itakapopita, wanaweza kupata lawama kutoka kwa waumini wao na kufananishwa na Mch. Kibwetele aliyehubiria na kuwaaminisha asiyoyaenenda yeye, na isipopita pia hawatabaki salama bali upande mwingine hasa CCM, itawalaumu kwa hamasa zao.
Kinachotakiwa kifanyike ni Katiba hiyo iwafikie haraka watanzania ili waisome na kuielewa kisha watoe maamuzi ya Ndiyo au Hapana.
Mwisho.